Kampuni ya mkonge ya Grosso ya nchini Uholanzi inatarajia kuwekeza Shilingi bilioni 132.8 kwa ajili ya kilimo na viwanda vya zao hilo.
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo Nuradin Osman alisema kuwa amebaini uzalishaji wa mkonge nchini hauna ufanisi kama unavyotakiwa kulingana na hali ilivyo duniani.
Alisema bado kuna pengo kubwa la uzalishaji, faida ndogo kwa wakulima, teknolojia hafifu, wawekezaji na wadau wengine katika sekta hiyo.
“Hali hiii haiwezi kuvutia soko la kimataifa jambo ambalo linaathiri uchumi wa nchi,” alisema.
Alisema uwekezaji wao unakusudiwa kuwa katika vipindi viwili ukiwa na lengo la kufufua zao hilo lililokuwa moja ya mazao makubwa ya biashara nchini.
Alisema “kiasi cha dola milioni 5.7 kitaingizwa kwenye ukuzaji wa zao la mkonge kwa kuanzisha viwanda vya kuchakata mkonge vitakavyoongeza thamani”.
Alisema kampuni itaanzisha mikakati ya kuunganisha wazalishaji ambao ni wakulima na wateja duniani ambapo kampuni itatoa dola 700,000 katika awamu ya kwanza.
Taarifa kutoka shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) zinaonyesha uzalishaji hautoshi hivyo kuna haja ya kuwa na uzalishaji zaidi.
Alieleza kuwa “Utekelezaji wa awamu ya pili utakuwa pamoja na kuanzisha mfumo wa kuongeza thamani katika sekta. Kampuni inalenga kuongeza thamani ya zao la mkonge kwa kuzalisha vileo, vyakula vya wanyama na sukari itokanayo na mkonge na kemikali inayozalisha nishati”.
.