Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ileje Joseph Mkude na timu ya wataalamu wa masuala ya kilimo mkoani Songwe kutembelea mashamba ya migomba na kufanya utafiti kuhusu mbegu bora ya migomba inayofaa kulimwa katika eneo hilo. Mama Samia amesema hayo baada ya kutembelea kijiji cha Sange na kujionea shughuli mbalimbali za kilimo wilayani hapo.
Makamu huyo amewataka wataalamu kufanya utafiti ili kupata aina nzuri ya mbegu itakayowasaidia wakulima wa eneo hilo kuondokana na kilimo cha migomba ya asili ambayo haina tija kwa uzalishaji na badala yake waanzishe kilimo cha migomba ya kisasa kitakachowasaidia kujiingizia kipato.
Aidha Mama Suluhu amesema utafiti huo unapaswa kujikita katika kuangalia aina ya mbegu za migomba inayolimwa, matatizo yake sambamba na kutafuta suluhisho ili kukuza uzalishaji katika zao hilo.
“Nimepita kote nimeona mnalima mazao mbalimbali lakini migomba ndio zaidi ambayo imezaa ndizi ndogo ndogo. Ninamtaka Mkuu wa wilaya pamoja na timu yake msaidie wakulima hawa waondokane na kilimo hiki”. Amesema Mama Suluhu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ileje amesema wameshaanza kutekeleza agizo hilo la kuhakikuisha wataalamu wa kilimo wana watembelea wakulima na kuwapa mbinu bora za uzalishaji wa kilimo cha migomba.