Shlingi bilioni 10.5 zitatumika katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa ukarabati wa Skimu ya Umwagiliaji Masimba katika Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida.
Mradi huo, unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, unalenga kuongeza tija ya kilimo kwa wakulima wa eneo hilo na kuboresha maisha ya zaidi ya watu 24,000 kutoka vijiji vya Masimba, Urughu, Mlandala, Mang’ole, na Ujungu.
Akizungumza katika Hafla ya kukabidhi eneo la mradi kwa mkandarasi iliyofanyika katika Kata ya Urughu, Waziri wa Fedha na Mbunge wa Iramba Magharibi Dkt. Mwigulu Nchemba amesisitiza kuwa hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Kilimo, chini ya uongozi wa Waziri Hussein Bashe, zinaimarisha kilimo cha kisasa na kuleta mapinduzi katika sekta hiyo, ambayo ni mhimili wa uchumi wa wananchi wengi nchini.
Dkt. Nchemba ameongeza kuwa mradi huo ni mfano wa jinsi serikali inavyotekeleza dira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya kilimo na hasa kilimo cha umwagiliaji, ili kuhakikisha uzalishaji endelevu na maendeleo ya jamii za vijijini.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Miundombinu Raphael Laizer, alifafanua vipengele vya mradi ambavyo ni pamoja na ukarabati wa bwawa na sehemu ya utoro wa maji, kuondoa mchanga na tope ndani ya bwawa ili kuongeza ujazo wake kwa mita za ujazo 250,000, ujenzi wa mfereji mkuu wa mita 200 kwa kiwango cha zege na ujenzi wa mifereji ya upili yenye urefu wa mita 9,254 kwa kiwango cha zege.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda, amesema mradi huu ni hatua kubwa inayojibu kilio cha muda mrefu cha wakulima wa eneo hilo kwa kutatua changamoto za upatikanaji wa maji ya uhakika kwa kilimo.
Skimu hiyo itakuwa na eneo la ekari 1,800 za umwagiliaji, ambapo wakulima watazalisha mazao ya mpunga na mbogamboga kwa wingi, hatua inayotarajiwa kuongeza mapato na kuboresha hali ya maisha.