Home KILIMOKILIMO UFUNDI Bilioni 65.16 kutumika mradi wa umwagiliaji

Bilioni 65.16 kutumika mradi wa umwagiliaji

0 comment 219 views

Takribani Tsh bilioni 65.16 zitatumika katika mradi wa ujenzi wa bwawa na skimu ya umwagiliaji wa Bonde la Luiche, mkoani Kigoma lenye ukubwa wa hekta 3000.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameshiriki katika kukabidhi mradi huo Julai 21, 2024 kwa mkandarasi M/S CRJE (East Africa) LIMITED ya Dar es Salaam.

Waziri Bashe amesema mradi huu ni muhimu ambao utanufaisha wananchi wa kata za Kagera, Simba na Mungonya katika Mkoa wa Kigoma.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.

Akitoa salamu za Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mkurugenzi Mkuu Raymond Mndolwa ameeleza kuwa mradi una gharama za Shilingi Bilioni 65.16 ambapo utahusisha ujenzi wa bwawa, mfereji mkuu wa kuingiza maji, uchimbaji wa mitaro ya kutoa maji katika mashamba, ujenzi wa barabara za mashambani, nyumba za watumishi, ofisi za wahandishi pamoja na ujenzi wa ghala na kusimika mashine ya kukoboa mpunga.

“Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imejipanga na tuko tayari kuhakikisha wananchi wa Bonde la Luiche wananufaika na mradi huu.

Tunampongeza sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kukuza kilimo cha umwagiliaji,” amesema Mndolwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, CGF (mstaafu) Thobius E. M. Andengenye amesema zaidi ya Shilingi Bilioni 60 zilizotengwa kwa ajili ya mradi huu ni hatua muhimu ya kuwajali wananchi wa Luiche na Kigoma kwa ujumla.

“Nikupongeze Waziri Bashe kwa kutafsiri maoni ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha ndoto ya mradi huu inaanza kutekelezwa,” amesema CGF Andengenye.

Ng’enda Kirumbe ambae ni Mbunge wa Kigoma Mjini ametoa shukran kwa Wizara ya Kilimo kwa kuleta mradi huo ambao umekuwa unazungumziwa tangu Uhuru.

“Mradi huu unakuja kututhibitishia sisi na vizazi vyetu mkono kwenda kinywani na kuongeza mzunguko wa fedha kupitia miradi wa kilimo cha umwagiliaji,” amesema Kirumbe.

Mkoa wa Kigoma una zaidi ya hekta 120,000 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo eneo linalomwagiliwa ni hekta 9,070 kukiwa na mabonde na skimu 59.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter