Home KILIMOKILIMO UFUNDI Vijana 150 wapata vitendea kazi vya kilimo

Vijana 150 wapata vitendea kazi vya kilimo

0 comment 21 views

Jumla ya vijana 150 wanaoshiriki kwenye mnyororo wa thamani katika Sekta ya kilimo wamenufaika na mradi wa Feed the Future Tanzania kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kwa kupewa vitendea kazi.

Vijana hao ni kutoka katika halmashauri ya Chunya, Mbeya vijijini na halmashauri ya Mbarali mkoani Mbeya.

Hafla hiyo imefanyika Septemba 17, 2024, mkoani Mbeya ambapo vifaa vya umwagiliaji (irrigation kits), pump za maji, vifaa vya kufugia pamoja na vifaa vya kutotoleshea mayai viligawiwa kwa vijana walioshiriki na kupata mafunzo mbalimbali.

Baadhi ya vijana wakipokea vitendea kazi vya kilimo

Mradi una lengo kuboresha mazingira ya kisera pamoja na kujenga uwezo na uelewa wa kupata mitaji na masoko ya bidhaa zao ambapo jumla ya vijana 100 wamefanikiwa kupata namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN) na vijana 57 kupata leseni za biashara.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amehudhuria hafla ya ugawaji wa vitendea kazi kwa vijana hao ambapo ameishukuru USAID kwa kuwekeza katika kilimo nchini kupitia vijana ikiwa ni njia ya kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amewekeza kupitia programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) katika kuhakikisha kilimo kinakua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Silinde ametoa rai kwa USAID kutanua wigo katika kuwafikia vijana wengi nchini, na kuwataka wanufaika wa mradi huo kutumia vifaa walivyokabidhiwa ipasavyo katika kukuza uchumi wao binafsi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Baadhi ya vijana wakipokea vitendea kazi vya kilimo

Naye mwakilishi wa USAID nchini, Joyce Mndambi ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa inaotoa katika kufanikisha mradi huu hapa nchini unaotekelezwa katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Morogoro, Unguja na Pemba.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter