Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka wananchi hasa wakulima wa korosho kutokuwa na hofu kwani korosho zao zote zitanunuliwa. Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha korosho cha Terra alipokuwa njiani kwenda jijini Dodoma na kueleza kuwa, serikali kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko itanunua korosho zote na hakuna korosho ambazo zitaachwa.
Waziri Mkuu amesema kuwa bodi hiyo inaendelea na zoezi la kufanya thamini na kujiridhisha kama korosho walizopokea zimezalishwa nchini na pamoja na kuangalia viwango vya ubora na baada ya kujiridhisha, taratibu za malipo hufanyika.
“Lengo la serikali ni kuhakikisha mkulima ananufaika na ndipo Rais Dk. John Magufuli alisitisha ununuzi baada ya kuona wakulima wanataka kudhulumiwa”. Amesema Waziri Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa pongezi kwa uongozi wa kiwanda hicho kwa jitihada wanazofanya kuunga mkono harakati za Serikali kukuza uchumi kwa kupitia sekta ya viwanda. Kwa upande wake, Meneja Utawala wa kiwanda hicho Peter Ngwale amesema uwezo wao ni kubangua tani 6,000 za koroshokwa mwaka na hadi sasa, tayari wamebangua tano 3,000.