Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameshauri wafanyabiashara kusambaza mbolea haraka iwezekanavyo ili wakulima waweze kuzipata kwa wakati kwani msimu wa kilimo tayari umeanza. Waziri Hasunga amesema hayo alipotembelea kampuni ya utengenezaji na usambazaji wa mbolea ya Yara Tanzania Ltd jijini Dar es salaam ambapo ametoa wito kwa taasisi zinazohusika na kupakua mizigo bandarini kufanya kazi ya hiyo kwa haraka ili mbolea ziwafikie wakulima kwa wakati. Waziri huyo ameeleza kuwa, sio jambo jema mbolea inayotakiwa kuwa mashambani kwa wakulima katika msimu huu wa kilimo kuendelea kukaa bandarini kwa zaidi ya wiki moja.
“Kadri mbolea inavyochelewa kuwafikia wakulima itasababisha kuongezeka kwa gharama zisizo na tija kwani atakayeumia ni mkulima jambo hili halipaswi kutazamwa kama jambo la kawaida badala yake wahusika wote watekeleze majukumu yao ipasavyo. Wakulima wengi vijijini hawajui mambo ya kukaa muda mrefu kwa mbolea bandarini wao wanachokijua serikali inatakiwa kuwapatia mbolea msimu wa kilimo unapofika, na mbolea inahitajika haraka kwani kilimo cha Tumbaku kinaendelea na tayari malalamiko yameanza” Amesema Waziri Hasunga.
Kwa upande wake, Meneja wa kampuni hiyo Tanzania na nchi jirani ya Rwanda, William Ngeno amesema kampuni ya Yara inalenga lengo kutoa huduma bora kwa wateja wao kupitia wataalamu wake. Aidha, Ngeno amempongeza Waziri huyo wa kilimo kwa kutembelea kampuni hiyo na kujionea inavyofanya kazi.