Serikali imesema ipo mbioni kuanzisha chaneli ya Kilimo kupitia Television ya Taifa (TBC) ambayo itatoa taarifa za mazao, elimu ya kilimo na kanuni bora za kilimo, maeneo ya uwekezaji pamoja na fursa mbalimbali zilizopo kwenye kilimo.
Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amesema hayo February 23, 2022 Jijini Dar es salam wakati akizindua kipindi maalum cha ‘Kilimo kwanza’ kitakachokuwa kinarushwa na kituo cha Televisheni cha TVE.
Kipindi hicho kina lengo la kuhamasisha kilimo miongoni mwa vijana na kutoa taarifa muhimu za kilimo.
Mavunde amesema “nawapongeza sana TVE kwa wazo hili la kuamua kuunga mkono jitihada za serikali za kukuza kilimo nchini.
Kipindi hichi kitasaidia sana kuhamasisha matumizi ya sayansi na kanuni bora za kilimo ili wakulima wetu walime kwa tija.”
Ameeleza kuwa kipindi hicho pia kitakuwa kinaongeza taarifa na maudhui ya kilimo ambayo yatarushwa kupitia TBC kwenye chaneli ya kilimo ambayo serikali inatazamia kuianzisha hivi karibuni.
“Chaneli hiyo itakayojikita kutoa elimu kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ikiwa ni pamoja na mafunzo ya kanuni bora za kulima na matumizi sahihi ya pembejeo kwa wakulima” Alisema Mavunde.
Afisa Mtendaji Mkuu ambae pia ni mmiliki wa EFM & TVE Francis Sizza maarufu Majizzo amesema lengo la kipindi hicho kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza kilimo.
Amesema wamejipanga vyema kuhakikisha wanawahamasisha vijana wa vijijini na mijini kushiriki katika kilimo ikiwemo wasanii wakubwa wa muziki na filamu nchini kama sehemu ya kampeni ya kunufaika na mpango wa serikali wa Building a better tomorrow _Toboa na Kilimo.