Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na zoezi la upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Skimu na Mabwawa, Visima virefu na Mabonde mbalimbali ya Umwagiliaji.
Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde amesema kuwa Serikali imetenga fedha kwa mwaka 2023/2024 kupitia mpango wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika kutekeleza ujenzi wa skimu na mabwawa hayo likiwemo Bonde la Mto Manongi linaloanzia Mkoani Shinyanga hadi katika Mkoa wa Singida.
Naibu Waziri Silinde amesema hayo leo February 9, 2024 wakati wa kipindi cha maswali na majibu Bungeni, jijini Dodoma akijibu swali la mbunge wa Jimbo la Bukene Selemani Zedi kuhusu mpango wa Serikali katika kufufua Skimu za Umwagiliaji za Ikindwa, Malolo na Nhalanga-Bukene ili zifanye kazi kwa tija.
Aidha, Silinde ameeleza kuwa Serikali imeazimia kuhakikisha kuwa inaongeza uzalishaji wa mazao ambayo yamekua yakiiwakilisha nchi kutokana na kupatikana kwa wingi nchini tofauti na upatikanaji wake katika Mataifa mengine.
Amesema katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 Serikali imepanga kuyatangaza mazao yatakayoingia katika Soko la Bidhaa la Tanzania.
“Serikali kupitia soko la bidhaa inaendelea kutoa elimu kwa wakulima na wadau kuzalisha kwa tija na kuuza katika soko rasmi, kwa maana ya Soko la Bidhaa Tanzania ambalo linawakutanisha wanunuzi wakubwa wa nje na wa ndani na kuwapatia bei zenye ushindani,” amesema Silinde.
Amesema Serikali imelenga kuanzisha Kituo rasmi cha Intelijensia na Kanzidata ya Mazao na Masoko ya Kilimo (Agriculture Marketing and Intelligence and Data Center).
Kituo hicho kitawezesha upatikanaji wa taarifa za masoko kwa wakati, kutoa mafunzo ya Kilimo Biashara kwa Maafisa Ugani na wakulima na kuendelea kufungua masoko mapya katika nchi mbalimbali za kufanya tafiti za mahitaji kwa nchi nzima.