Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa agizo kwa warajis wasaidizi wa mikoa pamoja na maafisa ushirika wa halmashauri za wilaya nchini kukutana na wadau wa vyama vya msingi vya zao la kahawa na kujadili upya tozo zilizopo katika zao hilo. Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na warajis wasaidizi na maofisa ushirika wa halmashauri za wilaya zinazozalisha mazao makuu ya biashara ambayo ni chai, pamba, tumbaku, kahawa na korosho.
Waziri Mkuu ameeleza kuwa tozo nyingi za sasa hazipo kwa mujibu wa sheria na zinawekwa na vyama vya msingi kuwanyonya wakulima badala ya kuwainua. Amedai kuwa tozo nyingi hazina uhalali na huwekwa na AMCOS na sio vyama vikuu. Ameagiza majadiliano kufanyika ili kuangalia namna ya kuongeza uzalishaji wa mazao hayo na vilevile kufuatilia maagizo aliyotoa katika ziara yake mikoani.