Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Kufaulu darasani ni Kufaulu maisha?

Kufaulu darasani ni Kufaulu maisha?

0 comment 39 views

Swali hili limekuwa likiulizwa kwa muda mrefu huku wengine wakikubali kuwa ukifaulu darasani basi umefaulu maisha kwa ujumla na wengine wakiamini kuwa hakuna uhusiano kati ya vitu hivyo viwili kwani wapo watu ambao wana maisha mazuri tu japokuwa hawakufanya vizuri darasani.

Ni kweli kuwa kuna waliotumia ubunifu, vipaji na ujuzi wao kujenga maisha mazuri lakini haimaanishi kuwa elimu haina umuhimu. Mchango wa elimu upo pale pale, hivyo kama umepata nafasi ya kusoma ni bora kuitumia vizuri ukajiongezea maarifa kisha ukatumia ubunifu na ujuzi wako binafsi kujiweka katika nafasi nzuri zaidi. Unaweza kujiuliza kwa soko la ajira lilivyo hapa nchini, mtu asiye na vyeti vya kudhibitisha elimu aliyonayo anaingiza kipato sawa na yule aliyesoma na kumaliza? Ukiwa unaomba kazi vipaumbele vipo vipi? Utakubali kuingiza kidogo kuliko yule mwenye elimu zaidi?

Kwa mazingira yetu hapa nchini ni kwamba, kufaulu darasani kunasaidia kwa kiasi fulani. Ni kweli kuwa nafasi nyingi za ajira zinaangalia ujuzi na ubunifu alionao muombaji kazi lakini hiyo haimaanishi kuwa kiwango chake cha elimu na ufaulu hakina thamani. Vijana wengi wamekuwa wakikosa watu sahihi wakuwapa ushauri hivyo wengine wamekuwa wakijikuta wakiachana na masomo na kujikita katika miradi mingine ili kujiingizia kipato lakini hata hivyo wasifanikiwe.

Wapo wengine ambao wanaamini kabisa kuwa hakuna ulazima wa kutumia gharama nyingi na muda mrefu darasani kama moja ya changamoto kubwa ambayo wahitimu wanakutana nayo wakiingia rasmi katika ulimwengu wa ajira ni kuwa mjuzi wa kazi hiyo kwa miaka kadhaa. Ni taasisi chache zana zinakubali kuajiri vijana waliotoka chuo moja kwa moja. Sasa kundi hili la watu wanapata wapi ujuzi? Hapa ndio wengine wanaona kabisa hakuna maada ya kuwekeza sana katika elimu kama bado utahangaika kusaka ajira.

Hapa ndipo tunapoweza kusema kuwa mfumo wetu wa elimu unafeli. Kwanini wanafunzi wasipatiwe ujuzi na kufundishwa na kuangalia uhalisia wa kile wanachosomea badala ya kusoma tu vitabu kila siku? Kwanini programu zisiwekwe vyuoni kuwatayarisha na maisha halisi baada ya kuhitimu? Masomo pekee hayatoshi. Inabidi kuwe na utaratibu ambao utawaruhusu wanafunzi na vijana kwa ujumla kuwa na elimu, ujuzi, kutumia ubunifu wao na kuwa na utayari wa kutumia yote hayo kwa pamoja kufaulu maisha.

Hii haimaanishi kuwa wale ambao hawakusoma hadi ngazi za juu kabisa walikosea, hapana. Tujifunze pia kutoka kwako. Watu hawa wana uzoefu wa muda mrefu ndio maana wana mafanikio hivyo tunapaswa kujifunza kutoka kwao pia. Hakuna ambae hataki kufanikiwa katika maisha yake, kinachotakiwa ni kutumia nafasi uliyonayo na kujifunza zaidi kutoka waliofanikiwa. Ni vizuri kuomba ushauri pale unapohitaji, kufanya utafiti kabla ya kufanya maamuzi na kuwashirikisha wengine kwani mawazo ya mtu mmoja pekee hayatoshi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter