Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imenunua tani 160 za korosho zilizo na thamani ya Sh. 550 milioni kutoka kwa wakulima wilayani Tunduru mkoani Ruvuma ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli la kutaka serikali inunue korosho hizo kufuatia hali ya kusuasua iliyokuwepo kwa wanunuzi. Fedha hizo zimetolewa kwa wakulima 534 wilayani humo ikiwa ni sehemu ya malipo ya korosho kwa msimu wa mwaka huu ambapo malori ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) tayari yameanza zoezi la kuchukua korosho hizo kwa ajili ya kubangua.
Mkuu wa wilaya hiyo Juma Homera amesema jumla ya magari kumi ya jeshi tayari yamewasili katika eneo hilo kwa ajili ya kubeba korosho zilizonunuliwa na serikali kupitia benki ya kilimo.
“TADB imefanya utaratibu mzuri kuhakikisha kila mkulima anapata fedha yake kulingana na mzigo wake na bei ya korosho iliyopangwa ya Sh. 3,300 kwa kilo, tunashukuru zoezi hili limekwisha salama na sasa tunapakia”. Amesema Homera.
Homera ameongeza kuwa wakulima wa zao hilo wilayani humo walionyesha kukata tamaa kufuatia kukosa wanunuzi kwa bei ya kuanzia Sh. 3,000 na kwamba, hatua iliyochukuliwa na serikali imewapa matumaini ya kuendelea na kilimo hicho.
“Wakulima kuwapo katika vyama vya ushirika imesaidia kuwa na msimamo na kuondoa adha ya wakulima kuuza korosho holela kwa walanguzi kwa kukosa fedha za kujikimu baada ya kukosa soko la mazao yao”. Ameeleza Homera.