Mkuu wa wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani Filbeto Sanga amesema serikali itawachukuliwa hatua za kisheria walanguzi wa zao la korosho watakaobanika wanarubuni wakulima kutouza korosho kwa serikali na badala yake kuwauzia wao. Sanga amesema hayo katika kikao cha Baraza la Madiwani Mkuranga na kueleza kuwa, wapo walanguzi ambao tayari wameshawasili vijijini na kuwalaghai wakulima kuwauzia korosho kwa gharama ya Sh. 4,090 kwa kilo moja badala ya Sh. 3,500 ambayo ni bei iliyopangwa na serikali.
“Hatutavumilia kuona walanguzi wakiingia vijijini kuwarubuni wakulima wawauzie korosho kilo moja Sh. 4,000”. Amesema Mkuu huyo wa wilaya.
Aidha, Sanga amewataka wakulima kutokubali kuuza korosho walizonazo kwa walanguzi kwani serikali ndio pekee inayonunua zao hilo. Mkuu huyo wa wilaya pia ameonya kuwa, walanguzi watakaokamatwa watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.