Na Mwandishi wetu
Rais wa jukwaa la wanawake wanaounda Jukwaa la Wakulima Wadogo nchini, Bi Eva Mageni ameitaka serikali kuongeza bajeti ya sekta ya kilimo ili wakulima wapate uwezo wa kuzalisha kwa wingi zaidi na kulisha viwanda.
Asilimia zaidi 70 ya watanzania wamejiajiri katika kilimo hivyo endapo serikali itaendelea kutenga bajeti ndogo kwenye sekta hii, ukweli ni kwamba azma ya serikali ya kufikia uchumi wa kati haitofanikiwa.
Bi. Eva amedai kuwa kama serikali ina nia ya dhati ya kubadilisha Tanzania hadi kufikia kuwa nchi ya viwanda, ni lazima bajeti ya kilimo iongezwe kutoka asilimia 4.6 iliyopo sasa hivi hadi kufikia asilimia 10 hivyo kuwapa motisha wakulima, ambao ndiyo wazalishaji wa malighafi kuwa na vitendea kazi vya kutosha.
Mbali na hayo, ameomba serikali kuhakikisha kila kijiji kinapelekewa maofisa ugani ili wakulima kote nchini wasaidiwe pale wanapokumbana na changamoto yoyote.