Na Mwandishi wetu
Baada ya Bodi ya Kahawa (TCB) kuunda sheria iliyowavua jukumu la kusimamia uzalishaji wa zao hilo nchini, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Charles Tizeba amesema sheria hiyo iangaliwe upya.
Waziri Tizeba ameamuru Mwanasheria wa bodi hiyo, Engarasia Mongi kwenda jijini Dar es salaam mara moja na kushirikiana na wanasheria wa wizara yake ili kubadili sheria hiyo. Kwa sasa jukumu la uzalishaji wa kahawa limeachwa kwa halmashauri za wilaya ambazo waziri huyo amedai zina mazao mengi ya kusimamia.
Awali majukumu ya bodi hiyo yalikuwa ni kusimamia sekta ya kahawa na kuratibu majukumu shirikishi ya wadau wa kahawa, ikiwemo uzalishaji. Hadi kufikia Septemba mwaka huu, mwanasheria wa TCB anatakiwa kuwa amewasilisha mswada ili bodi hiyo iongezewe jukumu la kusimamia uzalishaji wa kahawa.
Akiwa katika eneo la ushughuliaji sampuli za kahawa, Waziri wa Kilimo pia ameitaka bodi hiyo kuja na suluhisho la kudumu kudhibiti uvushaji haramu wa kahawa kwenda nchi jiarani na pia ameshauri bodi kutafuta mbinu sahihi za kuhakikisha vyama vya ushirika mkoani Kagera vinanunua kahawa kwa bei ya juu kama zinavyofanya kampuni za Uganda.