Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya umeme hasa katika maeneo ya vijijini ambapo gharama ya kuunganisha na kuweka umeme ni Sh. 27,000 katika vijiji vyote ambavyo vimepitiwa na mradi wa REA. Waziri Kalemani ametoa ushauri huo wakati akizindua umeme katika kijiji cha Kikumbaitale wilayani Chato ambapo ameeleza kuwa, serikali imejipanga kuipeleka nchi katika uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda, ambapo amewataka wananchi wa Chato kuanzisha mashine za kukoboa na kusaga pamoja na kufanya biashara mbalimbali ikiwemo biashara za saluni kwani uwepo wa umeme huo ni fursa kubwa kwa wananchi kufungua miradi mbalimbali itakayowasaidia kuingiza kipato.
“Lakini pia niwaaambie fungueni na saluni kwani umeme huu muutumie kujiongezea kipato ambacho kitakuwa chachu ya kujiletea maendeleo katika eneo lenu”. Amesema Dk. Kalemani.
Aidha, Waziri huyo amewapongeza viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kazi nzuri wanazofanya kwa kushirikiana na Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA) huku akisisitiza kuwa wataendelea kufanya kazi kwa bidii na kutembelea vijiji mbalimbali hapa nchini ili kukagua maendeleo ya mradi na kuhakikisha maeneo yaliyo ndani ya mradi yanapata umeme kwa wakati.