Bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Puma Energy Tanzania Limited leo imemkabidhi Rais Dk. John Magufuli gawio la kiasi cha Sh. 9 bilioni kiasi ikiwa ni sehemu ya gawio la bilioni 18 kwa mwaka 2017 pamoja na mwanahisa Puma Investment Limited waliopata pia bilioni 9, ikiwa ni gawio la asilimia 50 kwa kila mwanahisa yaani Puma Energy Limited na serikali ya Tanzania kupitia msajili wa hazina, Wizara ya Fedha.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja Mkuu, Meneja Uendeshaji wa kampuni hiyo Lameck Hiliyai amesema kutokana na uendeshaji na utendaji mzuri, gawio la kampuni hiyo limekuwa hadi kufikia asilimia 100 ikilinganishwa na gawio la mwaka 2015 na kwa asilimia 29 ikilinganishwa na gawio la mwaka 2016.
Hiliyai amesema hadi mwishoni mwaka jana Puma iliweza kuingiza faida yenye jumla ya kiasi cha Sh. bilioni 31 kabla ya kodi, na kuwekeza kiasi cha Sh. 9 bilioni kununua na kuendeleza miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo viwili vya mafuta jijini Dodoma, ikiwa ni katika kuiunga mkono serikali katika juhudi zake za kuhamia Dodoma.
“Ukuaji huu unaendana sambamba na mikakati ya kampuni kwa kuhakikisha kampuni inaendelea kukua, kutengeneza faida, kukuza ajira nchini, kuchangia pato la taifa kupitia kodi na kuendelea kuiunga serikali mkono katika kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo”. Amesema Hiliyai.