Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya amesema kufuatia jitihada za serikali ya awamu ya tano kuimarisha uchumi kupitia viwanda, takribani viwanda 3,504 vimeanzishwa nchini hadi kufikia Desemba 2018. Mhandisi Manyanya amesema hayo bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge Ussi Salum Pondeza wa Chumbageni aliyeuliza ni viwanda vingapi vimeanzishwa tangu serikali ya awamu ya tano ianze utekelezaji wa mpango wa kuimarisha uchumi wa kati wa viwanda.
“Kati ya viwanda hivyo 3,504 vilivyoanzishwa, vinajumuisha viwanda vidogo sana 2,500, viwanda vidogo 943, viwanda vya kati 51 na viwanda vikubwa 10”. Ameeleza Mhandisi Manyanya.
Mbali na hayo, Naibu Waziri huyo amesema Wizara imekuwa ikishirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina kufanya tathmini ya viwanda 156 vilivyobinafsishwa na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa kwa viwanda 68 ambavyo havijaendelezwa.
Aidha, Mhandisi Manyanya ameeleza kuwa, kwa mujibu wa hali ya uchumi ya mwaka 2017, sekta ya viwanda imechangia asilimia 5.5 katika pato la taifa ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 0.6 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2016.