Home VIWANDAMIUNDOMBINU Usafiri wa anga unavyokuza uchumi

Usafiri wa anga unavyokuza uchumi

0 comment 108 views

Imeshuhudiwa serikali ya awamu ya tano ikitekeleza moja ya ilani zake za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa kuchukua hatua kadhaa katika kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambalo hapo awali lilikuwa katika hali mbaya ya uendeshaji. Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imekuwa ikifanya maboresho kadhaa ya utoaji wa huduma za anga ikiwa ni pamoja na ununuzi wa ndege mpya nne ndani ya muda wa miaka miwili na nusu.

Katika sherehe za kupokea ndege mpya aina Boeing 787-8 Dreamliner zilizofanyika hivi karibuni, Rais Magufuli alidai kuwa serikali ya awamu ya tano imedhamiria katika kuhakikisha inafufua Shirika la Ndege Tanzania kwa kiwango cha Juu huku ikitarajiwa kuanzisha safari za nje ya nchi za ukanda wa Asia na Uingereza.

Rais Magufuli pia  alizungumzia mafanikio ya shirika hilo tangu ununuzi wa ndege mpya na kudai kuwa, idadi ya abiria wanaosafiri kupitia ndege hizo imekuwa ikipanda kila mwezi kwa zaidi ya ilivyotegemewa hapo awali. “Tangu tumeongeza ndege 3 mpya aina ya Bombardier Q400 biashara ya ATCL imeongezeka, Shirika letu lilikuwa linasafirisha abiria 4,000 tu kwa mwezi lakini sasa linasafirisha abiria 21,000 na ndege zinatua katika vituo 12.” alisema Rais Magufuli.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli aliweza kuweka bayana namna ndege hiyo itakavyosaidia kukuza shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja kuwavutia watalii sambamba na kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali.

Usafiri wa Anga ni moja kati ya Usafiri wa haraka na wa uhakika, hivyo ununuzi wa ndege mpya unatarajia kuleta mabadiliko makubwa katika kukuza uchumi, hasa kuelekea katika azma kuu ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati. Usafiri wa anga unao mchango mkubwa katika kukuza na kuimarisha uchumi kwa sababu zifuatazo:

  1. Usafiri wa anga unasaidia kukuza shughuli za utalii- Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa katikia sherehe za kupokea ndege mpya, takribani asilimia 70 ya watalii wanaoingia nchini wamekuwa wakitumia usafiri wa ndege na hivyo kusaidia kukuza uchumi.
  2. Usafiri wa anga unatoa fursa za ajira. Kupitia maendeleo ya usafiri wa anga serikali imeweza kutoa ajira mbalimbali kwa wazawa na wasio watanzania,katika vitengo mbalimbali kama vile watoa huduma, wahandisi, na marubani.
  3. Usafiri wa Anga unasaidia katika kukuza biashara za ndani na nje ya nchi. Ndege inasaidia kusafirisha watu na mizigo kwa wafanyabiashara kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kwa haraka zaidi. Shughuli za kibiashara zinaporahisishwa, zinasaidia mapato na uchumi wa nchi kuongezeka na kuimarika zaidi.
  4. Usafiri wa anga unasaidia kuongeza pato la taifa. Kupitia makusanyo ya mauzo ya tiketi, kodi inayokatwa kwenye tiketi serikali inaongeza kiasi cha makusanyo ya ndani ya nchi. Makusanyo hayo ndio huelekezwa kwenye huduma za kijamii, ujenzi wa miundombinu, kutoa elimu bure, kutoa huduma za kiafya n.k

Hivyo basi ni dhahiri kuwa dhamira ya serikali katika kukuza sekta ya usafiri wa anga ni njema kwani lengo kubwa ni kuongeza mapato ya nchi na kuhakikisha sekta zinazotegemea usafiri huo kwa asilimia kubwa kama utalii, biashara na uchukuzi zinaimarishwa kwa kuwepo uhakika wa usafiri.nkupitia mapato yanayokusanywa, taifa linaweza kufaidika na kusaidia utekelezaji wa miradi mingine ya kimaendeleo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter