Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya Petroli hapa nchini zitakazotumika kuanzia leo Jumatano Februari 05, 2025 kwa rejareja na jumla.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei ya petroli kwa rejareja katika Jiji la Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 0.957, dizeli kwa asilimia 2.18 na mafuta ya taa kwa asilimia 1.25.
Hii ikiwa na maana kuwa sasa wanunuzi wa mafuta kwa bei ya rejareja katika Jiji la Dar es Salaam watanunua lita moja kwa Sh2,820 kwa petroli, dezeli Sh2,703 na mafuta ya taa kwa Sh2,710.
Bei hizo ni kutoka Sh2,793 kwa bei ya petroli ndani ya jiji la Dar es Salaam kwa Januari mwaka huu, dizeli Sh2,644 na mafuta ya taa kwa Sh2,676.
Aidha, taarifa hiyo inawaelekeza wafanyabiashara wa rejareja na jumla wanatakiwa kuuza mafuta kwa bei zilizoidhinishwa na EWURA pekee na yeyote atakayekiuka agizo hili atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.