Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi William Lukuvi amewataka wananchi wa Kata ya Migori kutosita kuwafichua wavuvi haramu ambao wamekuwa wakivua samaki katika Bwawa la Mtera, kinyume cha taratibu na kanuni zilizowekwa na wizara hiyo ili kulinda maliasili ya bwawa hilo linalozalisha pia umeme wa gridi ya taifa.
Akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi mavazi ya kujiokoa kwenye maji yapatayo 100, yaliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi kavu na Majini (SUMATRA) kwa ajili ya kuwasaidia wavuvi katika shughuli zao, Lukuvi amesema atashirikiana na mamlaka husika kwa ajili ya kufanya operesheni ya kuwatafuta na kuwafichua wahalifu.
Soma Pia Wavuvi kukopeshwa
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Sumatra, Dk. John Ndunguru na Mkurugenzi Mkuu Gilliard Ngewe wamewashukuru wakazi wa kata ya Migori kwa msaada waliotoa kwa wenzao waliopatwa na maafa wilayani Chato mwaka jana kutokana na mvua na kuongeza kuwa msaada wa mavazi hayo ni moja ya fadhila ambazo serikali imewarudishia wananchi hao.