Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba ili sekta ya mafuta na gesi iweze kufanikiwa, serikali inapaswa kutambua gharama za miradi na kuweza kukokotoa faida ya rasilimali hizo kwa manufaa ya taifa. Makamba ambaye alifungua mkutano wa wadau wa mafuta na gesi ikiwa alimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amedai kuwa, uwezo huo ndio utakaoweka wazi faida inayoweza kupatikana na kunufaisha taifa.
Makamba amefafanua kuwa hiyo inatokana na uvunaji wa rasilimali hizo kuwa suala geni katika nchi za Afrika, ambazo kutokana na matumizi ya teknolojia duni, wawekezaji wengi ni wageni kutoka mataifa ya Ulaya. Waziri huyo ameongeza kuwa suala la kufahamu gharama halisi za miradi zinazotumiwa na wawekezaji walio na teknolojia ya uchimbaji na miradi mikubwa inayohitajika inabaki kuwa nyenzo muhimu ya kukokotoa namna ya kupata faida.
Aidha, Waziri Makamba amesema kuwa serikali imekuwa ikifanya harakati za kubadili Sheria na kuweka mipango na mikakati itakayohakikisha matumizi ya rasilimali ya gesi na mafuta yanakuwa na manufaa kwa nchi.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), Abdulsamat Abdulrahim amesema kongamano hilo la pili linahusisha wadau wote walio na miradi ya mafuta na gesi hapa nchini na kuongeza kuwa, wadau hao kutoka maeneo mbalimbali duniani wamekusanyika kujua fursa zilizopo na zinazoendelea kupatikana ili kujua namna ya kukuza uwekezaji.