Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Prof. Sylvester Mpanduji amesema ikiwa mikoa itasimamia utekelezaji wa programu ya Wilaya Moja Bidhaa Moja (ODOP), uzalishaji wa bidhaa za mazao ya kilimo pamoja na mifugo utaongezeka kwa kuwa utekelezaji huo umeshaanza kuonyesha mafanikio kwenye baadhi ya mikoa.
“Programu hii imechochea mazao ya kilimo na mifugo kuongeza uzalishaji wa bidhaa kupitia viwanda vilivyopo katika wilaya husika na huchagiza maendeleo katika ngazi ya wilaya na hatimaye taifa kwa ujumla. ODOP imeweza kutekelezeka katika mikoa mbalimbali ikiwemo Singida, Mbeya, Dodoma, Manyara na Morogoro katika kuzalisha bidhaa zinazotokana na mazao ya kilimo na mifugo kama vile alizeti, mahindi, mpunga na mazao ya mbogamboga. Programu hii itachochea ukuaji wa uchumi na kuleta maendeleo ya haraka katika wilaya husika kupitia mapato yatakayopatikana kutoka katika viwanda vyao hali itakayochochea miundombinu na mahitaji muhimu kupatikana kwa wakati”. Ameeleza Mkurugenzi huyo.
Aidha, Prof.Mpanduji ametoa wito kwa wananchi kuanza kutumia programu ya ODOP kwani mchango wake katika kukuza uchumi ni mkubwa.
“SIDO inaendelea kusimamia programu hii na jukumu lake kubwa ni kuhakikisha viwanda vinaanzishwa na kukua kutoka viwanda vidogo na hatimaye kufikia viwanda vikubwa vinavyoweza kujiendesha na kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi”. Amesema.