Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti wakiongozwa na Mwenyekiti wao, George Simbachawene wametembelea kiwanda cha kuzalisha transfoma cha TANELEC jijini Arusha kwa ajili ya ukaguzi wa masuala mbalimbali ikiwemo uwezo wa uzalishaji wa transfoma, ili kuhakikisha kuwa nchi inajitosheleza na vifaa vya umeme.
Wakiwa katika ziara hiyo ambayo waliambatana na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani pamoja na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wajumbe hao wamepongeza kiwanda hicho kwa kuzalisha transfoma takribani 14,000 kwa mwaka japokuwa mahitaji ya transfoma nchini kwa mwaka ni 10,000.
Pamoja na hayo, wajumbe hao wametoa pongezi kwa serikali kufuatia uamuzi wake wa mwaka 2017 ambao ulielekeza miradi yote ya umeme kutumia vifaa vya umeme vinavyopatikana ndani ya nchi ili kuharakisha utekelezaji wa miradi.
Aidha, wajumbe hao wametoa wito kwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo kuongeza uzalishaji na kutafuta masoko mengine ukiachana na ile ya miradi ya umeme ya ndani ya nchi pekee.
Kwa upande wake, Waziri Kalemani amesema serikali ilisitisha kuagiza vifaa vya umeme nje ya nchi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme.