Home VIWANDAUZALISHAJI Serikali yasimamisha uchimbaji madini mto Zila, Mbeya

Serikali yasimamisha uchimbaji madini mto Zila, Mbeya

0 comment 19 views

Serikali imesimamisha shughuli za uchimbaji madini zilizokuwa zikifanywa na kampuni ya G & I Tech Mining Company Ltd kwa kipindi cha masika na pia mpaka pale tathmini ya kitaalam ya mazingira itapokamilika juu ya shughuli za uchimbaji madini kwenye Mto Zila.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesimamisha shughuli hizo Desemba 30, 2024 katika kijiji cha Ifumbo, Wilayani Chunya alipotembelea eneo la leseni ya mwekezaji ambalo lilivamiwa na wananchi na kusababisha mgogoro mkubwa na uharibifu wa mali za mwekezaji huyo.

“Tumetembelea maeneo yote mawili, na sote tumejionea hali halisi ya mazingira. Ni dhamira na maelekezo ya Rais Dkt. Samia S. Hassan kuona shughuli zote za kiuchumi hususan za madini zinafanyika kwa utulivu bila kuleta migogoro na pasipo kuathiri mazingira ya eneo shughuli zinapofanyika.

Nimesikiliza hoja za wananchi juu ya uharibifu wa mazingira ya Mto Zila,serikali itaunda timu ya wataalamu kufanya tathmini ya kina ya mazingira juu ya athari zinazoweza kutokea wakati wa uchimbaji wa madini na kwasasa shughuli zote za uchimbaji madini zisimame kipindi hichi cha masika kama ilivyoelekezwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira_(NEMC).

Wizara ya madini kwa kushirikiana na watalaam wa mazingira, wataalam wa Mkoa na wananchi katika muda mfupi ujao inakwenda kuunda timu ya pamoja ya kufanya tathmini ili itueleze kitaalam iwapo shughuli hizi zinaweza kuendelea kufanyika pasipo athari kwenye mazingira ya mto Zila.

Nitumie fursa hii kuwataka wananchi wote kuacha vitendo vya uvunjifu wa amani na kujichukulia sheria mkononi, tunalaani kitendo cha kuvamia na kuharibu mali za mwekezaji,” amesema Waziri Mavunde

Awali, akitoa maelezo ya utangulizi, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Batenga alishukuru ujio wa Waziri wa Madini na kusisitiza kwamba sasa anaona mwanga ambao unakwenda kuleta suluhisho la kudumu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter