Tangu mwaka 2017 serikali ya Tanzania ilianza kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki nchini kwa sababu ya athari ambazo mifuko hiyo imekuwa ikileta kwa mazingira na viumbe hai kwa ujumla, lakini wananchi wamekuwa wakipuuzia katazo hilo, sababu kubwa ikiwa bei nafuu inayovutia wateja na wafanyabiashara kuitumia.
Aprili 9 mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kuwa mifuko ya plastiki inatakiwa kuacha kuzalishwa na kutumika kuanzia Juni Mosi mwaka huu. Agizo hilo limewapa fursa wenye viwanda vya plastiki na wengine kuchangamkia fursa ya kutengeneza mifuko mbadala ambayo ni salama zaidi.
“Kuanzia sasa tunatoa fursa ya viwanda kubadilisha teknolojia, wauzaji kuondoa mzigo uliopo, Ofisi ya Waziri wa Nchi, Makamu wa Rais itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hili kuwa la nguvu ya kisheria. Tunachukua hatua hii kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki”. Alisema Waziri Mkuu.
Tangu zuio hilo, viongozi mbalimbali wametoa maoni yao, pia wenye viwanda wameeleza maoni yao kuhusu maamuzi hayo. Serikali kwa kuonyesha msisitizo wamekuwa wakijitahidi kuwakumbusha wananchi wote nchini kupitia ujumbe mfupi (SMS) unaoelezea kukatazwa kwa mifuko ya plastiki kwa wazalishaji, wauzaji na watumiaji huku ikionya kwamba atakaYekutwa anatumia mifuko hiyo kuanzia tarehe 1 Juni atawajibishwa kisheria aidha kwa kutoa faini au kufungwa.
Ni kweli kwamba maamuzi haya yanaweza kuwa yamewaathiri watu wengi lakini kwa upande wa pili mazingira yatakuwa na muonekano mpya na salama, pia ni wakati muafaka kwa watanzania kutumia ipasavyo malighafi zilizopo nchini kwa mfano pamba, mabaki ya miti n.k kujitengenezea kipato na kuchochea maendeleo.
MIFUKO MBADALA
Mifuko mbadala inaweza kutengenezwa kwa malighafi nyingi zilizopo nchini. Baadhi ya mifuko hiyo ni kama ifuatavyo:
Mifuko ya karatasi
Karatasi hutokana na miti. Hivyo basi wazalishaji wanaweza kujikita katika utengenezaji wa mifuko kwa kutumia makaratasi kwani nchi yetu kwa ujumla ina misitu mingi, na pia kuna programu za kupanda na kukata miti nyingi. Serikali inaweza kuwahamasisha wananchi kujikita katika kupanda misitu zaidi ili kuwe na mzunguko nikimaanisha mazingira hayaharibiki kwa sababu ya ukataji wa miti na wazalishaji hususani wa mifuko ya karatasi wanaendelea kujipatia malighafi.
Vikapu
Vikapu hutengenezwa kwa miti au matawi, imekuwa kawaida sana kuona barabarani hasa zinazoenda mikoani wajasiriamali wadogo wamepanga vikapu vya kila aina na ukubwa kwa ajili ya kuuza. Wazalishaji wakipewa nyenzo na mitaji zaidi itasaidia kuongeza bidhaa hizo sokoni, na pia itawasaidia kupata kipato zaidi huku wakilinda mazingira na wakati huo huo kuongeza mapato.
Hivyo serikali inatakiwa kutafuta namna ya kuwaunganisha watengenezaji wa vikapu hivi ili waweze kuzalisha zaidi vikapu hivyo na kukidhi mahitaji ya wananchi huku wakileta maendeleo kwa ujumla.
Mifuko ya pamba
Pamba inazalishwa nchini, na mifuko yake huwa imara. Ili kuwarahisishia wazalishaji, serikali ingefanya makubaliano na wakulima wa pamba ili waweze kufanya biashara pamoja yaani, wakulima wa pamba wauze pamba kwa wazalishaji wa mifuko ili wazalishaji waweze kutengeneza mifuko kwa gharama nafuu.
Mifuko ya nguo
Mifuko hii mara nyingi hutengenezwa kwa ajili ya watalii. Wazalishaji wanatakiwa kuchangamkia fursa hii kwa kutengeneza mifuko inayotokana na vitambaa vya nguo kwa mfano vitenge kuwauzia na wananchi wa kawaida kwa lengo la kujipatia wateja zaidi na kuongeza kipato.
Itakuwa rahisi kama wazalishaji wa mifuko watapata malighafi ndani ya nchi na kwa bei nafuu. Hii itawasidia kuzalisha mifuko zaidi na katika ubunifu kwa kila aina hivyo kuepukana na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu ukosefu wa mifuko ya kubebea bidhaa au vifaa.