Na Mwandishi wetu
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametaka wahusika katika viwanda vya umma ambavyo vilibinafsishwa kuhakikisha vinafanya kazi na kutumia malighafi kutoka ndani ya nchi yatokanayo na mazao ya kilimo kwani kufanya hivyo kutatoa ajira za moja kwa moja na hata zile ambazo sio za moja kwa moja.
Majaliwa amesema hayo akiwa mkoani Morogoro alipotembelea viwanda vya Philip Morris Tanzania (PMT) pamoja na kiwanda cha mafuta ya kula cha Moproco. Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya tano imeandaa mikakati itakayoboresha mazingira ya kibiashara hapa nchini ili kuendelea kukuza uchumi.
Mbali na hayo, Waziri Mkuu ametaka wawekezaji walio na nia ya kuwekeza nchini kufanya hivyo kwani serikali inaendelea kuboresha mazingira katika sekta ya uwekezaji hivyo ameshauri serikali katika ngazi ya mkoa wa Morogoro kusimamia masuala ya uwekezaji na kulinda mafanikio yake.
Naye kwa upande wake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amesema ni jukumu lake kuhakikisha viwanda vya umma vilivyobinafsishwa vinafanya kazi kama inavyotakiwa.