Home BENKI Benki zifanye hivi kuwateka vijana

Benki zifanye hivi kuwateka vijana

0 comment 141 views

Utandawazi na uvumbuzi wa teknolojia za kisasa vimeendelea kuchangamsha taasisi za fedha hususani benki kwenda na wakati ili kutimiza mahitaji ya wateja wao. Vijana ni sehemu ya wateja ambao benki zinatakiwa kuwahamasisha zaidi kuendelea kutumia huduma kwa ajili ya masuala mbalimbali ya kifedha kwa sababu hawataki kufanyiwa maamuzi ya kifedha bali wanataka kufanya maamuzi yao wenyewe, wanataka kupata taarifa kwa urahisi zaidi kupitia mtandao bila kwenda benki moja kwa moja.

Inaelezwa kuwa asilimia 34 ya vijana hawafurahishwi na hali yao ya kifedha huku asilimia 60 wakielemewa na madeni. Taasisi za kibenki zinaweza kutumia nafasi hiyo kuwafikia vijana lakini kwa namna ambayo itawafanya watilie mkazo na si kupuuzia matangazo yanayohusu huduma za benki kama ambavyo wamekuwa wakifanya.

Vijana wanataka huduma kwa uharaka, urahisi na uwezo wa kujihudumia. Vilevile wanapendelea zaidi huduma ambayo inapatikana saa na mahali popote hivyo benki zinatakiwa kuhakikisha huduma zao zinapatikana kwa urahisi, katika vifaa vya kisasa vya kielektroniki. Kwa mfano CRDB kupitia huduma ya Sim Banking hupendelea kutuma ujumbe kwa wateja wao kuhusu huduma wanazozitoa. Hili ni jambo zuri na linaweza kuwa limewahamasisha vijana wengi. Ni muhimu kwa benki kufanya utafiti kila wakati ili kwenda na wakati na kuhakikisha kuwa wanapata mrejesho mzuri.

Benki zinatakiwa kutambua kuwa vijana sio waoga wa hatari, au teknolojia zinazoendelea kuundwa bali wao ni waoga wa kutopata vitu wanavyotaka ndani ya muda na kwa urahisi. Hivyo benki zinashauriwa kuwekeza katika teknolojia za kisasa zaidi ili kuhakikisha huduma zinawafikia vijana kwa urahisi zaidi, kwani idadi ya vijana ni kubwa sana hivyo kwa kuwafikia kwa urahisi mamilioni ya vijana kutanufaisha zaidi benki.

Kwa vijana, suala la kumbukumbu ni muhimu zaidi kuliko kitu kingine na ndio maana utaona kila siku mamia ya vijana wanatuma picha au video mbalimbali katika mitandao ya kijamii kuhusu uzoefu waliopata katika tukio fulani au kwa kwenda mahali fulani. Benki zichukue fursa kama hizo kuwavutia vijana kwa mfano hivi karibuni Wasafi Festival inaanza na hili ni tamasha linalopendwa zaidi na vijana hivyo benki yoyote inaweza kuwahamasisha vijana kufungua akaunti katika benki husika, ambapo baada ya kufungua watu 10 au 50 watapata zawadi ya tiketi ya tamasha hilo, vijana hata ,1000 wanaweza kufungua akaunti katika benki hiyo ili waweze kujipatia tiketi. Na kupitia mambo kama hayo kutaleta muamko kwa vijana kuhusu benki husika na mambo mazuri wanayoweza kuyapata katika benki hiyo.

Ili kuhamasisha vijana, benki zinatakiwa kujihusisha na vijana kwa ukaribu zaidi kwani vijana hufurahishwa zaidi na watoa huduma ambao wanawaelewa. Pia kwa kuweka huduma zao kwa mfano kutangaza huduma za elimu ya fedha, mikopo, uwekaji wa akiba n.k katika mtazamo ambao utawagusa vijana kutumia huduma za benki.

Watu maarufu na wenye ushawishi ni moja ya njia ya kuwahamasisha vijana kutumia huduma za benki. Standard Chartered ilizindua mfumo mpya ambao unawawezesha wateja wake kupata huduma zaidi ya 70 za kujihudumia na kumtangaza msanii maarufu wa muziki hapa nchini Vanessa Mdee kama mwakilishi wa huduma hiyo katika promosheni mbalimbali.

Bado sekta ya benki ina kazi kubwa ya kuwahamasisha vijana watumie huduma zao lakini kwa kutumia mbinu sahihi, taasisi hizi zina uhakika wa kuwa na mahusiano mazuri na vijana kwa sasa na siku zijazo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter