Home BIASHARA Wajasiriamali wa kati wameongezeka kwa kiasi kikubwa nchini

Wajasiriamali wa kati wameongezeka kwa kiasi kikubwa nchini

0 comment 106 views

Jumanne Rajabu Mtambalike ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Sahara Ventures inayojishughulisha na kuunganisha wajasiriamali wa kati na makampuni ya uwekezaji nje ya nchi kidigitali.

Kampuni hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2016, ni atamizi ya kusaidia makampuni madogo madogo kuwa tayari kukutana na wawekezaji mbalimbali kwa kuwapa ubunifu, ushauri na teknolojia.

Mtambalike ambae pia ni mjasiriamali wa kati kwa kutumia mitandao, anasema tangu kuanzishwa kwa Sahara Ventures wameweza kufikia makampuni takribani 2000 kupitia tamasha la Sahara Spark ambalo hukusanya watu kutoka Tanzania na nchi mbalimbali barani Afrika.

Tamasha hili, hufanyika kila mwaka likiwa na lengo la kukusanya wajasiriamali pamoja na vijana kuwajengea uwezo katika sekta mbalimbali za uwekezaji ikiwemo kilimo, fedha pamoja na afya.

Mtambalike anaeleza kuwa wajasiriamali wa kati wameweza kuongezeka kwa asilimia kubwa kutokana na kukua kwa teknolojia pamoja na fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo matamasha ambayo yanawapa fursa ya kueleza biashara zao na maonyesho.

Anasema teknolojia pia inachangia sana kuongozeka kwa wajasiriamali kutokana na matumizi ya masoko ya kidigitali (Digital Marketing).

Anasema kupitia masoko hayo ya kidigitali wanaweza kuunganisha wajasiriamali wa kati na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali.

“Tunafanya kazi kwa njia ya mtandao ambapo tunawasaidia wajasiriamali ambao tayari wana biashara zinazoendelea kuwaunganisha na wawekezaji katika sekta husika. Hii imeleta mafanikio makubwa sana, imesaidia makampuni madogo kukua na kuongeza uwekezaji kwa kiwango kikubwa,” amesema Mtambalike.

Akizungumzia swala biashara ya mitandao Mtambalike amesema kwa jinsi teknolojia inavyokuwa kwa kasi ndivyo wafanyabiashara wengi wanavyotumia mitandao kukuza biashara.

“Biashara nyingi sasa zimehamia mitandaoni kutokana na kukua kwa teknolojia, na huku sasa ndipo kwenye fursa nyingi zaidi. Niwape wito vijana kujifunza jinsi ya kutumia mitandao hii kujipatia kipato kuliko kutumia mitandao kwenye mambo yasiyo na maana,” amesema Mtambalike.

Ameeleza pia kuwa wanashirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) katika kuwajengea uwezo vijana katika kazi za ubunifu na ujasiriamali.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter