Home KILIMO Wakulima 21,000 kunufaika na mradi wa Umoja wa Ulaya

Wakulima 21,000 kunufaika na mradi wa Umoja wa Ulaya

0 comment 202 views

Takribani wakulima wapatao 21,000 wa Zanzibar wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kukuza kilimo cha mbogamboga, mazao ya viungo na matunda kupitia mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) wenye thamani ya shilingi bilioni 14.

Akizungumza na maofisa wa Halmashauri ya Magharibi B unguja, Meneja utafiti wa mradi huo Ally Mbarouk alisema mradi huo wa miaka mine utanufaisha shehia 50 kutoka Unguja na Pemba.

“Mradi huu utatekelezwa katika wilaya tisa za Zanzibar, tano za kisiwa cha Unguja na nne Pemba,” alisema Mbarouk.

Alisema maeneo yote yamezingatia ushari wa wataalamu wa wizara ya kilimo.

“Mradi umelenga kuwakutanisha pamoja wadau wote wanaohusika na uzalishaji wa mazao mbalimbali, kuongeza ubora wa uzalishaji wa bidhaa za kilimo pamoja na kuongeza lishe na uhakika wa chakula kwa wakazi wa visiwani hapa,” alisema.

Aidha, mradi huo pia utaongeza thamani bidhaa zinazozalishwa na kuongeza masoko nje na ndani ya nchi.

Alibainisha kuwa tayari kupitia washirika wao kwenye mradi huo, taasisi ya kimataifa inayojihusisha na uhifadhi wa misitu (CFI) yenye makazi yake nchini Canada wamekusudia kukuza soko la bidhaa za Zanzibar kimataifa kwa lengo la kutoa fursa zaidi.

Afisa wa Masuala Mtambuka kutoka Baraza la Mji Kaskazini B, Nahla Mohamed alisema ujio wa mradi huo utakuwa mkombozi kwa wakulima visiwani humo.

Mazao ya viuongo ambayo yamepewa kipaumbele katika uzalishaji ni tangawizi, iliki, vanilla, pilipilimanga na pilipili hoho.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter