Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ameziagiza halmashauri zote kuwatengea wafanyabiashara wadogo wadogo (machinga), maeneo yanayofikiwa na watu ili waweze kunufaika na biashara zao, badala ya kuwapeleka katika maeneo ya mapori.
Akizungumza na Vijana katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza katika mkutano uliolenga kujadili fursa mbalimbali za kumkomboa kijana, Rais Samia amesema Serikali inajenga masoko na standi katika kila mkoa ili kutenga maeneo kwa ajili ya machinga waweze kufanya biashara bila kubugudhiwa lakini baadhi ya watendaji wamekuwa wakiwapeleka katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi.
“Lakini pia tumehimiza halmashauri kutenga maeneo maalum ambayo yanafikiwa na watu ili vijana hao machinga wakakae na wafanye biashara zao, pamoja na maelekezo hayo, juzi niliona pale Morogoro machinga wametengewa maeneo ya nje ya mji ambako watu hawafiki na kwa sababu hawauzi wamerudi maeneo waliyoondoshwa.
“Niliona mgambo wakiwavamia wakawapiga na kuharibu vitu vyao, nimesikitishwa sana na tukio hilo, na niseme hapa mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa eneo lile hawana kazi,” alisema Rais Samia.
Rais alisema ”kwa sababu kuna njia nzuri zaidi ambayo wangeitumia kusema nao na wakawaondoa kwa usalama lakini si picha ile nilioiona kwenye TV, kwa hiyo nakuagiza Waziri wa Tamisemi ulishughulikie suala hilo,”.
“Nanyi watoto wangu machinga nawasihi sana msitumiwe na wafanyabiashara wenye maduka, mnapochukua bidhaa zao na kuwauzia kumbukeni hamtoi risiti hivyo mnaikosesha serikali mapato maana fedha tunazopata kutoka kwa wafanyabiashara wanazolipa ushuru ndizo tunazozitumia kuwaboreshea maeneo ya kufanyia biashara pamoja na kutatua changamoto mbalimbali hivyo nawaomba msitumike kabisa,”alisema.