Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanza kuwasajili wamachinga waliopo katika Soko Kuu la Biashara Kariakoo.
Meneja wa Mkoa wa Kikodi wa Kariakoo Alex Katundu amesema tayari machinga 5273 wameshasajiliwa ili kuingizwa kwenye mfumo wa malipo ya kodi wa makadirio.
Katundu amesema “usajili huu unafanyika kwa kila machinga aliyepo Kariakoo kwa sababu tulibaini baadhi ya wafanyabiashara wengine sio waaminifu, haonekani akifanya biashara ila mizigo yake anaisambaza kwa machinga ili akwepe kodi”.
Amesema mamlaka hiyo inawasajili baada ya kujiridhisha kwamba wote wanaingiza mapato zaidi ya Sh milioni nne (4) kwa mwaka.
Usajili huo ulioanza Februari mwaka huu, unafanyika ikiwa ni utekelezaji wa tangazo la Kamishna wa TRA la Julai mosi mwaka huu, linaloagiza kila machinga kusajiliwa eneo hilo.
Katundu amesema baada ya kusajiliwa wote watakabidhiwa mashine za EFDs kwa ajili ya kushiriki kwenye ulipaji wa kodi ya makadirio.