Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Maagizo 6 Dira ya Maendeleo ya Taifa

Maagizo 6 Dira ya Maendeleo ya Taifa

0 comment 100 views

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Philip Mpango ametoa maagizo sita ya kuzingatiwa katika Maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Moja ya maagizo hayo ni kuimarisha uwezo wa uchumi uliopo na kulinda mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2025.

Ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati wa akizundua Mchakato wa Maandalizi ya dira mpya ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Amesema maandalizi hayo pia yazingatie matumizi ya fursa ambazo hazijatumiwa ipasavyo hadi sasa na kuzikamata fursa zinazochipukia huku akitolea mfano kilimo, mifugo na uvuvi, mazao ya misitu, uongezaji thamani ya mazao pamoja na uvunaji wa rasilimali za kimkakati na kujenga viwanda.

“Katika kilimo Tanzania ina fursa ya kuwa ghala la chakula katika Bara la Afrika na hata mashariki ya kati na duniani kama tukilenga uzalishaji mkubwa wa mahindi, ngano, shayiri, maharage ya soya, sukari, mafuta ya kupikia, korosho, matunda, mbogamboga na viungo ”, amebainisha Dkt. Mpango.

Amesema maamdalizi pia yazingatie suala la elimu, hususani elimu ya sayansi, elimu ya ufundi na ufundi stadi, utafiti na maendeleo na ubunifu ili kukuza ujuzi na uwezo wa nguvu kazi ya Taifa.

“Jambo la nne ni namna gani tutavutia na kuasili teknolojia ili kukuza tija katika sekta zote za uzalishaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi ikiwa ni pamoja na kuingia ubia wa kimkakati ili kuiwezesha Tanzania kuwapita washindani wetu katika kipindi kifupi”, ameeleza.

Amesema kubaini uhalisia wa rasilimali zote zitakazo hitajika kuwezesha utekelezaji makini wa Dira mpya na utekelezaji wa mipango, pamoja na kubainisha mfumo thabiti wa ufuatiliaji na tathimini kwa kuangalia vigezo mahsusi vilivyowekwa.

Amesema ni vema timu zilizoundwa zikajifunza kutoka katika nchi zilizoendelea kwa kasi kuanzia miaka ya 1960 hususan zile za Bara la Asia pamoja na kuangalia namna nchi nyingine zilivyoweza kujikwamua kutoka katika uchumi wa kati.
Dk Mpango ameeleza kuwa ni matumaini ya Serikali kuwa wananchi watapata nafasi ya kutoa maoni yao katika mchakato wa maandalizi ya Dira mpya ambayo inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii.

Soma: Wadau watakiwa kutoa maoni Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter