Serikali ya Tanzania imesema imedhamiria kufikisha watalii milioni tano na sekta hiyo kuchangia mapato si chini ya dola bilioni sita ifikapo mwaka 2025.
Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Saba ya Swahili International Tourism Expo – S!TE, 2023 yaliyofanyika Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
“Mmemsikia Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ameeleza vizuri na kusadifu namna ambavyo Ibara ya 68 ya Ilani yetu ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iivyotuelekeza ifikapo mwaka 2025 tunapaswa kuwa tumefikisha watalii takribani milioni tano.
Na sekta yetu ya utalii iwe inachangia mapato si chini ya dola bilioni sita,” amebainisha Waziri Kairuki.
Amesema kama Wizara watafanya kila linalowezekana kuhakikisha idadi ya watalii inaongezeka.
Ameeleza kuwa Serikali inakusudia kukuza utalii wa fukwe, mikutano pamoja na utalii wa kuvinjali kwa meli ikiwa ni mkakati wa kuongeza mazao mapya ya utalii nchini kwa ushirikiano baina ya Tanzania bara na visiwani.
Aidha, amesema Serikali inatambua wajibu huo na imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha uwepo wa mazingira yatakayopelekea utalii endelevu (sustainable Tourism).
“Ni kwa sababu hiyo Ripoti ya Baraza la Utalii na Masuala ya Safari Duniani (World Travel and Tourism Council, WTTC) ya Mwezi Mei, 2022, imeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 bora Duniani kwa uhimilivu wa maeneo yake kupokea watalii (sustainability).
Matunda ya hatua zinazochukuliwa na Serikali yanaonekana wazi. Leo hii pamoja na athari za UVIKO19, tunafurahi kwamba kasi ya kukua kwa sekta ya utalii wetu ni nzuri,” amebainisha Waziri Kairuki.
Waziri Kairuki ameongeza kuwa mafanikio hayo yamepelekea Sekta ya utalii kuchangia asilimia 25 ya fedha za kigeni, na asilimia 17.5 ya pato la taifa ambapo amesisitiza kuwa huo ni mchango mkubwa kwa uchumi wa nchi yetu.
Amesema sekta ya utalii inatoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa wananchi na kwamba Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba sekta hii inabaki kuwa imara na inazidi kukua.
Pia amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha miundombinu kama vile barabara, reli na viwanja vya ndege ili kuhakikisha wageni wanayafikia maeneo yote yenye vivutio vya utalii kwa urahisi.
Maonesho hayo yamekutanisha waoneshaji takribani 150 kutoka nchi mbalimbali na wanunuzi zaidi ya 71.