Home FEDHA TAMISEMI yaomba Sh Trilioni 10.125

TAMISEMI yaomba Sh Trilioni 10.125

0 comment 260 views

Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), taasisi zilizo chini yake, mikoa 26 ikijumuisha halmashauri 184 zimeomba Bunge kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 yenye jumla ya shilingi trilioni 10.125.

Kwa mwaka 2023/24, Ofisi ya Rais-TAMISEMI iliidhinishiwa bajeti ya trilioni 9.18.

Kati ya fedha hizo, trilioni 3.52 ni fedha za maendeleo na trilioni 5.65 ni za matumizi ya kawaida na hadi kufika Machi, 2024 ofisi imekusanya na kupokea trilioni 6.99 sawa na asilimia 76.18 ya fedha zilizoidhinishwa na kati ya hizi trilioni 4.47 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na trilioni 2.52 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikijumuisha trilioni 2.06 fedha za ndani na bilioni 456.39 fedha za nje.

Haya yamebainishwa Aprili, 16, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mohamed Mchengerwa wakati wa kuwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa na taasisi zake kwa mwaka 2024/25.

Amesema kati ya fedha zinazoombwa, zaidi ya trilioni 6.71 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida wakati zaidi ya trilioni 3.42 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo kati ya fedha hizo zaidi ya trilioni 2.27 ni fedha za ndani na trilioni 1.145 ni fedha za nje.

Aidha, Mchengerwa amesema katika mwaka 2024/25, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, taasisi zilizo chini yake, mikoa 26 ikijumuisha halmashauri 184 imepanga kukusanya maduhuli na mapato ya ndani jumla ya zaidi ya trilioni 1.60 ikilinganishwa na trilioni 1.14 iliyoidhinishwa mwaka 2023/24, ikiwa ni ongezeko la Shilingi bilioni 456.89 sawa na asilimia 39.93.

Amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 188.96 ni makisio ya kodi ya majengo ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI ambayo yatakusanywa na mamlaka za serikali za mitaa zilizopewa uwakala wa kukusanya kodi hiyo na kuwasilisha makusanyo hayo Mfuko Mkuu wa Serikali.

Sh. bilioni 55.42 ni mapato ya ndani ya taasisi wakati Sh. milioni 315.93 ni maduhuli ya mikoa na Sh. trilioni 1.35 ni za mapato ya ndani ya halmashauri.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter