Home FEDHAMIKOPO Watoa huduma ndogo za fedha wanolewa

Watoa huduma ndogo za fedha wanolewa

0 comment 24 views

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha warsha kwa watoa huduma ndogo za fedha kuhusu namna bora ya kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma na bidhaa za kifedha nchini.

Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo, Mkurugenzi wa Huduma Jumuishi za Fedha kutoka BoT Kennedy Komba amesema kuwa utatuzi wa malalamiko ni sehemu ya kulinda haki za mtumiaji wa huduma za fedha.

Amesema hiyo itasaidia kurekebisha mapungufu yaliyopo katika utoaji huduma za kifedha, kuwapa imani wateja kuhusu huduma na bidhaa hizo pamoja na kuboresha sifa ya watoa huduma hao kwa wateja wao.

“Utatuzi wa malalamiko ya haki za watumiaji wa huduma za kifedha unasaidia kurekebisha mapungufu na changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta hii na kuwaongezea sifa watoa huduma za kifedha,” amesema.

“Michakato imara ya utatuzi wa migogoro ya ndani (Internal Dispute Resolution) si tu inajenga uaminifu bali pia inatoa taarifa muhimu kwa wasimamizi wa sekta hiyo ili kuwasaidia katika utengenezaji wa sera kulingana na changamoto zilizopo,” amesisitiza Komba.

Pia, ameeleza kuwa Mfumo wa Utatuzi wa Malalamiko ya Kifedha (FCRS) uliyotengenezwa na Benki Kuu utasaidia kuhakikisha malalamiko ya wateja yanatatuliwa kwa ufanisi, uwazi na usawa.

Nao, washiriki wa warsha hiyo, wameishukuru BoT kwa kuandaa warsha hiyo na wameipongeza kwa kuzingatia usawa na kuhusisha pande zote mbili yaani watoa huduma za kifedha pamoja na watumiaji wa huduma hizo katika kutatua malalamiko ya wateja.

Warsha hiyo inatarajia kufikia tamati Septemba 20, 2024 ambapo itahusisha pia washiriki kutoka kwenye mabenki na watoa huduma za malipo wasiokuwa mabenki (non-bank service providers).

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter