Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Mtukufu Aga Khan wa IV afariki dunia akiwa na umri wa miaka 88

Mtukufu Aga Khan wa IV afariki dunia akiwa na umri wa miaka 88

0 comment 8 views

KIONGOZI Mkuu wa 49 wa Madhehebu ya Shia Ismailia na mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), Mtukufu Aga Khan, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88 jijini Lisbon, Ureno, Februari 4, 2025.

Mtukufu Aga Khan, anayefahamika kama Karim Al-Hussaini Aga Khan IV, alijulikana kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha ustawi wa binadamu kupitia miradi mbalimbali duniani.

“Katika maisha yake, Aga Khan IV alisisitiza Uislamu ni imani inayohimiza kujitolea, uvumilivu, na utu wa mwanadamu,” inasema taarifa rasmi kutoka Ureno.

Alizaliwa Desemba 13, 1936, Geneva, Uswisi, na alikulia Nairobi, Kenya. Alipata elimu katika shule ya Le Rosey nchini Uswisi na Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, ambako alisomea masomo ya Uislamu.

Baada ya kifo cha baba yake, aliacha ndoto zake za soka na masomo ya uzamivu ili kuchukua wadhifa wa Imamu wa 49 wa madhehebu ya Shia Ismailia.

Mtukufu Aga Khan IV alipokutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Octoba 2017. Picha |UN/Eskinder Debebe

Mbali na uongozi wa kidini, alihimiza maendeleo ya jamii kupitia sekta za afya, elimu, habari, utamaduni, na ustawi wa jamii.

Alianzisha miradi kama Shule na Chuo Kikuu cha Aga Khan, Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Aga Khan (AKFED), na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), ambao umeleta maendeleo katika afya, elimu, na uchumi, hasa Afrika Mashariki.

Nchini Tanzania, mchango wake unaonekana kupitia Mwananchi Communications Limited (MCL) na Hospitali za Aga Khan, huku nchini Kenya alianzisha Nation Media Group (NMG) na viwanda kadhaa.

AKDN imeleta mafanikio katika jamii barani Afrika, Asia, na Mashariki ya Kati kwa kusaidia maendeleo katika maeneo yaliyoachwa nyuma.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter