Kampuni ya Vertif imetambulisha vifaa vya kutunzia umeme maarufu kama UPS hapa nchini maalum kwa ajili ya taasisi kubwa na viwanda. Mfanyabishara mwenza wa kampuni hiyo Mihayo Willmore ameeleza kuwa UPS hizo zimefanyiwa maboresho na zimepewa uwezo wa kukabili dharura ambazo zinaweza kuleta hasara katika viwanda au taasisi kubwa.
Ameongeza kuwa walengwa wakubwa hivi sasa ni viwanda,taasisi za serikali, sekta ya afya pamoja na vituo vya kanzidata ambavyo vinahitaji umeme muda wote. Amesema vifaa hivyo vinaweza kusaidia katika kutoa huduma kwa wagonjwa na hata katika uzalishaji viwandani na vilevile vinatoa muda wa kutosha kwa wahusika kutafuta suluhisho la kudumu pale dharura inapotokea.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni hiyo ukanda wa kusini mwa Afika Johan Van Wyk amesema umeme ni changamoto kubwa katika nchi nyingi duniani hivyo vifaa hivyo vitakuwa msaada mkubwa na vitasaidia kuepusha madhara yanayotokana na ukatikaji umeme.