Mtendaji mkuu wa benki ya CBA Dk. Gift Shoko amesema japokuwa benki hiyo ilipitia wakati mgumu mwaka jana na hata kupata hasara ya zaidi ya Sh. 15 bilioni, hivi sasa benki hiyo ina mtaji wa zaidi ya Dola bilioni mbili za Marekani hivyo wapo imara katika utendaji na utoaji huduma.
Dk. Shoko ameeleza kuwa mtaji walionao hivi sasa unawaweka miongoni mwa taasisi imara zaidi za fedha hapa nchini na inawaondolea tishio la kufungwa kwasababu mtaji unajitosheleza, na vilevile wanao utaalamu na mipango endelevu ya biashara.
Mbali na hayo, Mtendaji huyo amesema CBA itaendelea kuwekeza katika teknolojia ili kuongeza ufanisi. Hadi kufikia Machi mwaka huu, benki hiyo imetoa mikopo ya zaidi ya bilioni 10 kwa wateja wa Vodacom M-Pawa.