Ni muhimu kuwa na akiba kwani husaidia pindi tatizo linapotokea ghafla. Mtu anayetumia mifumo rasmi ya kutunza fedha kama benki anakuwa katika nafasi nzuri siyo tu kutumia akiba yake pale uhitaji wa haraka ukitokea, lakini pia katika shughuli za kimaendeleo. Siyo watanzania wote hujiwekea mazoea ya kutunza fedha zao katika mabenki kutokana na sababu mbalimbali walizonazo. Makala hii inakusudia kueleza baadhi ya faida za kutunza fedha zako katika taasisi hizi kama ifuatavyo.
Kutunza fedha katika benki ni njia salama zaidi ya kulinda fedha zako. Kuna tofauti kubwa ya kuweka fedha nyumbani ambapo zipo katika hatari ya kuibiwa na hata kupata majanga kama moto. Kuwa na fedha nyingi pia kunahatarisha usalama wa raia kwani kumekuwa na taarifa kadhaa za matukio ya ujambazi sehemu mbalimbali kote nchini. Kupeleka fedha benki kunaondoa wasiwasi wa yote hayo kwani fedha zinakuwa katika ulinzi na usalama zaidi ukilinganisha na namna zinavyokuwa nyumbani.
Kutumia huduma za benki pia inarahisisha upatikanaji wa mikopo pale mtu anapohitaji. Hakuna benki ambayo itakupatia mkopo kama haujawahi hata kutumia huduma zao. Kuwa na akaunti ambayo inaonyesha matumizi ya mteja na kiwango cha fedha hivyo benki inapata urahisi pale mtu huyo anapohitaji mkopo kwani wanakuwa na rekodi za kifedha za mteja hivyo kupata uhakika kuwa mkopo utarejeshwa ndani ya wakati uliokubaliwa.
Faida nyingine za mtu binafsi au hata taasisi kuweka fedha benki ni kuongeza mtaji kwa kupata riba kulingana na muda ambao fedha hizo zinapokuwa benki. Fedha zilizotunzwa huongezeka kwa kiasi fulani kila baada ya muda uliopangwa hivyo mtumiaji anapata zaidi ya alichoweka, fedha ambazo anaweza kuzitumia kujiletea maendeleo zaidi katika biashara zake au shughuli zozote za kujiletea maendeleo.
Fedha zinapowekwa katika benki pia hunufaisha nchi yetu kwa ujumla kwani zinatumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu, afya, maji, ujenzi wa barabara na kilimo. Hivyo matumizi ya taasisi za kifedha husaidia nchi pia kuboresha huduma za kijamii ambazo watumiaji wa benki wananufaika nazo baadae.
Benki zinapaswa kuendelea kuboresha huduma kwa wateja wao lakini pia kuelimisha wananchi wengi zaidi kuachana na utunzaji usio salama na kuhamia katika huduma zao bora zaidi na za kisasa. Taasisi hizi zinapaswa kutumia mbinu kama mikutano, semina au matangazo ili kuwafikia watu wengi zaidi na kuhakikisha kuwa jamii ina uelewa mkubwa wa manufaa ya huduma za benki.