Home FEDHA Sherehe zisikuache maskini

Sherehe zisikuache maskini

0 comment 89 views

Imekuwa ni desturi yetu hapa nchini kwa watu kutumia gharama kubwa katika sherehe mbalimbali. Wahusika hutafuta huku na kule mpaka kuhakikisha kuwa yale yote yaliyolengwa yanafanikiwa. Ni jambo la heri kusherekea, hilo halina pingamizi lakini kwanini tunaenda nje ya uwezo wetu ili tu kutumia fedha zote hizo ndani ya siku moja? Haiwezekani kwa watu kufanya sherehe kwa kuangalia uwezo walionao? Kuna ulazima wa kuingia gharama kubwa ili tu kusherekea? Je, maisha baada ya sherehe yanakuwa vipi?

Ukweli ni kwamba kila mtu anatamani kufanya sherehe nzuri. Kila mmoja wetu anatamani kufanya vitu vikubwa katika siku hiyo muhimu lakini tunajipanga kiasi gani kupambana na hali ya maisha baada ya hapo? Kwanini kiasi fulani cha fedha hizo zisiwekezwe katika maisha ya baadae? Katika elimu? Kwa watoto na vitu vingine ambavyo bila shaka vina umuhimu mkubwa zaidi?

Sherehe na hafla mbalimbali sio kitu kibaya. Ni vizuri kukaa pamoja, kujumuika na kusherekea mafanikio mbalimbali tunayopata katika maisha. Tatizo ni pale ambapo gharama kubwa inatumika wakati inawezekana kabisa kufanya sherehe iliyo ndani ya uwezo wako kiuchumi. Fedha nyingine zingeweza kuelekezwa katika masuala ya kimsingi na kimaendeleo badala ya muziki, chakula na vinywaji pekee. Jamii yetu inapaswa kuangalia suala hili katika mtazamo tofauti na kujenga desturi ya kuwasaidia wapendwa wao kusonga mbele kimaisha mbali ya kuwafanyia sherehe za kifahari. Bila shaka hiyo itakuwa zawadi nzuri na yenye manufaa.

Itakuwa vizuri kama tukibadili mitazamo yetu katika masuala ya sherehe. Ni wakati wa kutumia fedha zinazopatikana kwa ustaarabu na busara. Hakuna umuhimu wa kufanya sherehe ya gharama wakati ungeweza kutumia kiasi fulani cha fedha hizo kujiendeleza. Bajeti zetu ziendane na hali yetu ya maisha ili kuruhusu watu waweze kuwa katika nafasi nzuri kiuchumi hata baada ya sherehe hizi kukamilika. Muda umefika sasa wa kubadilisha dhana ya kwamba ili sherehe iwe sherehe nzuri basi lazima gharama kubwa itumike. Badala yake, tujifunze kupangilia sherehe, tuwe makini katika bajeti na la muhimu zaidi, tufahamu kuwa kuna maisha baada ya sherehe.

Jambo la msingi kufanikisha sherehe ni uwepo wa ndugu, familia, marafiki na majirani kwani maana halisi ya sherehe ni kufurahia kwa pamoja  na wale unaowathamini. Kuna kila sababu ya kufanya sherehe kwa kuangalia uwezo ulionao. Gharama ya maisha zinaendelea kupanda kadri miaka inavyokwenda hivyo basi hamna haja ya kuingia gharama kubwa na kujirudisha nyuma kimaendeleo eti kwa sababu tu ni sherehe. Yapo mambo ya msingi zaidi ya kufanya katika maisha hivyo kuwa makini na maamuzi yako kwani yanaweza kukuletea madhara siku za mbele.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter