Home VIWANDA TRA yagundua njia mpya kukusanya kodi viwandani

TRA yagundua njia mpya kukusanya kodi viwandani

0 comment 105 views

Mamlaka ya Mapato Tanzania(Tra) imekuja na njia mpya ya kukusanya kodi nchini kwa kuwataka wafanyabishara wanaomiliki viwanda vinavyohusika na utengenezaji wa malighafi za kutengenezea pombe kali kutoa takwimu sahihi na inayoridhisha juu ya ukusanyaji kodi stahiki kupitia vinywaji hivyo.

Hayo yameelezwa na kamishna wa Kodi za ndani wa TRA Elijah Mwandumbya baada ya kutembelea kiwanda cha sukari kinachomilikiwa na Manyara Sugar Company Limited Mkoani Manyara.

Alisema utoaji takwimu huo utaipa TRA uwezo wa kufuatilia kwa ukaribu na kupata taarifa sahihi za kodi ili kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato.

“Tunafahamu kwamba Molasisi (Malighafi inayotokana na miwa baada ya kutengeneza sukari) ni bidhaa inayotumika kutengenezea pombe kali, hivyo takwimu zitatuwezesha kufuatilia wafanyabiashara wanaonunua bidhaa hiyo na kutengenezea pombe kali ili nasi tukadai kodi yetu na hatimaye ilete tija kwa taifa”. Alisema.

Naye mkuu wa mkoa wa manyara Alexander Mnyeti alisema kuwa mkoa wa Manyara wamejipanga katika kutekeleza mkakati wa kuongeza viwanda vikubwa na vidogo ili kuleta maendeleo kwa mkoa na taifa kwa ujumla, kwani itasaidia kuongeza wigo mpana wa ajira.

“Tunataka kuongeza viwanda vingi katika mkoa wetu ili serikali iweze kupata kodi zaidi na kuongeza mapato kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu. Alisema Mnyeti.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Manyara Sugar Company Limited Bwn. Pratap Sisulya alimshukuru Kamishna wa Kodi za ndani kwa kutembelea kiwanda hicho na kuahidi kutoa ushirikiano wa wa kutosha kwa TRA katika kuhakikisha kampuni hiyo inalipa kodi zote kwa muda mwafaka sambamba na kutoa takwimu sahihi za uzalishaji.

“Ni wajibu wetu kutoa takwimu sahihi kwa TRA pamoja na kulipa kodi kwa wakati.” Alisema.

Akielezea tathmini ya ulipaji kodi wa kiwanda hicho Mkurugenzi huyo alisema mwaka 2017/2018, Kampuni imelipa kodi takribani Sh.Bilioni 1 huku kiwanda hicho kikizalisha zaidi ya tani 4000 za sukari kwa mwaka. Aidha alisema kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikiajiri wafanyakazi wa muda wapatao 350 hadi 400 kwa siku

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter