Home KILIMO Kero hizi zitatuliwe kuinua kilimo

Kero hizi zitatuliwe kuinua kilimo

0 comment 87 views

Ni ukweli usiopingika kuwa asilimia kubwa ya chakula kinachozalishwa nchini kinatoka vijijini. Mkulima huyu anaamini kilimo ndio ajira pekee aliyotunukiwa hivyo nguvu yote amewekeza huko. Wakulima wengi vijijini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinasababisha mkulima kuendelea kuwa duni kutokana na namna ya uendeshaji wao wa kilimo kuendeshwa katika hali ya uduni sana.

Hizi hapa ni baadhi ya changamoto zinazowakabili wakulima katika maeneo tofauti hapa nchini.

Ukosefu wa zana bora za kilimo.

Wakulima wengi vijijini bado wapo nyuma katika teknolojia na zana duni zimeendelea kutumika katika uzalishaji na hivyo kupelekea uzalishaji mdogo wa mavuno. Mfano mpaka sasa asilimia kubwa ya wakulima wengi wanatumia jembe la kukokota pamoja na jembe la mkono. Hivyo wadau wa kilimo, sekta mbalimbali na serikali wana wajibu mkubwa wa kuwasaidia wakulima kuendana na mazingira ili kuongeza nguvu ya uzalishaji.

Ukosefu wa miundombinu.

Baada ya mavuno bado wakulima wameendelea kupata changamoto ya usafirishaji wa mazao yao, kutokana na vijiji vingi kukabiliwa na miundombinu mibovu na hivyo wanalazimika kuuza mazao yao kwa walanguzi kwa bei ya hasara. Mara nyingi walanguzi ndio wamekuwa wapangaji wa bei za mazao na sio wakulima wala serikali.

Uhaba wa wataalamu wa kilimo.

Tatizo hili ni kubwa sana maeneo ya vijijini kutokana na uhaba wa maafisa kilimo nchini. Bado katika utendaji, kuna changamoto katika namna ya maafisa hao kuwafikia wakulima kwa sababu baadhi ya maafisa wamekuwa wakishinda ofisini badala ya  kuzunguka vijiji mbalimbali kutatua kero za wananchi.

Uhaba wa elimu kwa vitendo (Shamba Darasa)

Kwa kawaida serikali ya kijiji au kata chini ya Afisa Kilimo inashauriwa kuwa na Shamba darasa. Shamba darasa ni shamba ambalo huandaliwa na wataalamu wa kilimo kwa ajili ya kuwafundisha wakulima juu ya mbinu bora za kuzalisha kuanzia kupanda hadi uvunaji. Mashamba haya ni machache sana nchini na wakulima wengi wamekuwa wakikosa elimu hii ya vitendo. Hii inatokana na baadhi ya maafisa kilimo kushindwa kutekeleza majukumu yako sambamba na kujua kuwa shughuli zao zimejikita mashambani na sio ofisini.

Ni jambo lisilopingika kuwa kilimo ni sekta yenye uwanja mkubwa wa ajira japokuwa wasomi wengi wamekuwa wakikimbilia fursa nyingine. Dhana hii inapaswa kupigwa vita kwani kilimo si kwa ajili tu ya mazao ya chakula bali kuna kilimo cha biashara ambacho kinahusisha uzalishaji wa malighafi, hivyo ni dhahiri kuwa endapo wadau wa kilimo, biashara, sekta binafsi za kifedha na kilimo wataamua kuwekeza hasa vijijini, vijana wengi watapata muamko mkubwa.

Serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa ili kuetlekeleza hili kupitia maonyesho ya kilimo ya Nanenane ambayo hufanyika kila tarehe 8 Agosti. Pia serikali imekuwa ikitoa tuzo kwa wakulima bora na wafugaji bora kikanda na kimkoa kila mwaka ili kuhamasisha uzalishaji zaidi katika kilimo.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter