Mkurugenzi Mtendaji wa jiji la Arusha, Dk. Maulid Madeni amesema jiji hilo limeweka azma ya kukusanya Sh. 30 bilioni kutoka Sh. 15 bilioni inayokusanywa hivi sasa kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato vilivyopo jijini humo. Dk. Madeni ameeleza nia hiyo katika semina ya kuwajengea uwezo maofisa maendeleo ya jamii wa kata zote za jijini humo na kufafanua kuwa, ili kufanikisha lengo hilo, maofisa hao kwa kushirikiana na maofisa biashara pamoja na watendaji wa kata na mitaa watatakiwa kupata idadi kamili ya wafanyabishara, viwanda pamoja na maduka.
Mkurugenzi huyo amedai kuwa vyanzo vingi vya mapato bado havijafikiwa kikamilifu lakini kupitia mkakati huo, vitaweza kufikiwa na hivyo kusaidia kuongeza mapato kwa maofisa hao. Dk. Madeni pia amesisitiza kuwa ili kuepuka udanganyifu wa aina yoyote, mashine za kisasa za EFD zitanunuliwa na kusambazwa kwa wakusanya mapato.
Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Maendeleo ya Jamii jiji la Arusha, Tajiel Mahega, amesema wamegundua matumizi ya jiji hilo ni makubwa ikilinganishwa na mapato hivyo wameamua kutoa elimu kwa maofisa maendeleo ya jamii ili kuongeza wigo wa ukusanyaji.