Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) Mhandisi Raymond Seya amesema shirika hilo lipo tayari kupokea uwekezaji wa viwanda vya aina zote kutokana na kuwa na umeme wa kutosha, bora na wa uhakika. Mhandisi Seya amesema hayo baada ya kufanya ukaguzi na kuangalia maendeleo ya mradi wa umeme wa Kinyerezi II jijini Dar es salaam.
“Mradi unafikia mwisho sasa, kwa sababu mashine zote zimeshafungwa na uwezo wa mashine hizi ni kuzalisha Megawati 240, tunamalizia mambo madogo madogo kama ujenzi wa barabara na kupaka rangi lakini pia kujenga ofisi za wafanyakazi. Tunataka kuwahakikishia wananchi uwekezaji huu mkubwa wenye thamani ya zaidi ya Sh. 750 bilioni zote zikiwa zimetolewa na serikali umekamilika na tayari umeingizwa kwenye Gridi ya taifa. Tunapenda kumshukuru sana Mhe. Rais wa serikali ya awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuridhia kufadhili mradi tunawahakikishia sera ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda itatekelezwa kikamilifu na sisi kama TANESCO tuko tayari kupokea uwekezaji wa viwanda vya aina zote”. Amesema Mhandisi huyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Kinyerezi II, Mhandisi Stephens S. A. Manda amesema miradi yote miwili (Kinyerezi I na Kinyerezi II) ni ya kimkakati na kwamba wakati mradi wa Kinyerezi II tayari umekamilika, mradi wa upanuzi wa Kinyerezi I, umefikia asilimia 70.