Benki ya Stanbic imezindua huduma mpya na ya kidigitali iitwayo “Uhuru Banking”. Jina ‘Uhuru’ likiwakilisha ofa za kipekee, ikiwemo; kutokuwa na makato ya kila mwezi katika akaunti, kadi ya VISA ya daraja la dhahabu ‘Gold visa debit card’ inayotumika hapa nchini na kimataifa. Wateja wa Uhuru Banking wanaweza pia kufanya miamala mbalimbali na kujihudumia wenyewe kupitia simu zao za mkononi.
Benki ya Stanbic iliamua kuboresha huduma hiyo ambayo mwanzo iligawanyika katika akaunti za daraja tatu tofauti, yaani, Silva, Dhahabu na Bluu (Silver, Gold na Blue). Uhuru Banking inaunganisha madaraja ya akaunti zote na kuwawezesha wateja kuwa na uhuru wa kufanya miamala yao kiurahisi kupitia mfumo wa kidigitali. “Uhuru banking ni matokeo ya maoni ya wateja kuhusiana na huduma na bidhaa zetu. Wateja wetu ni kiini cha kila jambo tunalolifanya hivyo tumejikita katika kuhakikisha wanaendelea kifedha” alisema Mkuu wa kitengo cha wateja binafsi na kibiashara wa benki ya Stanbic, Brian Ndadzungira.
Watanzania wanahitaji huduma ambazo zinaendana na maisha ya sasa. Kupitia Uhuru banking wateja wanaweza kupata huduma mahususi za kifedha zinazoendana na mahitaji yao. “Pendekezo hili limelenga kuleta maendeleo kwa watanzania na kuwasaidia kufanyikisha malengo yao ya kifedha” aliongeza Brian.
Kumekuwa na mabadiliko ndani ya sekta ya benki nchini Tanzania na kutokana na uzoefu wa zaidi ya miaka ishirini nchini Tanzania, Stanbic Bank inaendelea kutoa huduma bora na mahususi zinazozingatia matakwa ya wateja wao.