Home FEDHA Alichosema Rais Magufuli kuhusu mapato,kodi na mazingira ya biashara

Alichosema Rais Magufuli kuhusu mapato,kodi na mazingira ya biashara

0 comment 113 views

Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameeleza kuwa Tanzania haifanyi vizuri katika ukusanyaji mapato ikilinganishwa na baadhi ya nchi barani Afrika kulingana na pato lake la taifa. Rais Magufuli amesema hayo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na TRA pamoja na wakuu wa mikoa kutoka nchi nzima ambapo amesema kuwa Tanzania ndiyo nchi yenye wastani mdogo wa kukusanya kodi , ambapo inakusanya asilimia 12 ya kodi, ikiwa na takribani walipa kodi milioni 2 kati ya watanzania milioni 54.

Aidha, Rais Magufuli amezitaka TRA pamoja na Wizara ya Fedha kutoza kodi ya nyumba ya Sh. 10,000 kwa nyumba za kawaida, Sh. 20,000 nyumba za ghorofa zilizopo wilayani na vijijini na Sh. 50,000 kwa nyumba kubwa. Ametaka tozo hizo kuzingatia hati ya kiwanja badala ya idadi ya nyumba kwenye kiwanja.

“Katika makadirio ya kodi ya nyumba, wapo wanaokadiriwa hadi Sh. Milioni 2 au Sh. Milioni 3. Nyinyi wakuu wa mikoa ni mashahidi, mtu amejenga nyumba kwa gharama halafu mnatoza kodi hizo, halafu hata bomba la maji hamjaleta. Watanzania tuko Milioni 55 lakini idadi ya nyumba zinazolipiwa kodi ziwe Milioni 1.9. Natoa wito kwa TRA na mamlaka nyingine za mapato hakikisheni mnatengeneza mifumo rahisi kwa wawekezaji na mpunguze vikwazo. TRA tumeshindwa hata kurasimisha sekta ambayo si rasmi ambayo ni asilimia 70, tunakusanya kwenye sekta rasmi ambayo ni asilimia 30 pekee, tunashindwa kukusanya mapato kwenye sekta isiyo rasmi, niseme ukweli hatufanyi vizuri kabisa”. Amesema Rais Magufuli na kuongeza:

“Yapo matatizo katika TRA yenyewe, kwenye mgawanyo wa watendaji katika maeneo mbalimbali. Kuna baadhi ya wafanyakazi wanapigwa vita, wanaondolewa na kuwekwa wengine kwa upendeleo. Lipo tatizo la kubambikizia watu kodi kupitia mfumo wa kukadiria. Mtu ana biashara ndogo anakadiriwa kodi kubwa, mwisho wake anafunga biashara, sasa hapo TRA mmepata faida au hasara? Wengine wanafunga biashara na kwenda kufungua upya maeneo mengine. Mazingira ya kufanyia biashara nchini bado ni tatizo. Usafirishaji, utitiri wa taasisi za usimamizi na tozo, ucheleweshaji bandarini, tatizo la umeme, kutumia muda mrefu kupata vibali vya biashara. Hatufanyi vizuri katika kuvutia wawekezaji”.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter