Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) jijini Arusha Isaya Shekifu amesema mfuko huo unatoa wito kwa wanachama wa vyama vya msingi vya ushirika wa mazao kujiunga na bima ya afya ili kupata matibabu bora ikiwa ni mpango wa serikali ya awamu ya tano kuwa, ifikapo 2020 idadi kubwa ya wanachama iwe tayari imejiunga na mfuko huo.
Meneja huyo amesema Ushirika Afya ni mpango ulioanzishwa na serikali kwa lengo la kutoa huduma ya bima ya afya kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika vya msingi kwa kuanzia na mazao matano. Mazao hayo matano ya kimkakati ni pamoja na korosho, pamba, chai, kahawa na tumbaku.
Shekifu amesema mkulima anapaswa kulipa Sh. 76,800 ukiwa ni mchango wake kwa ajili ya kupata Ushirika Afya ambapo ataweza kupata huduma ya matibabu kwa mwaka mzima na pia ataruhusiwa kuwakatia mzazi, mwenza, mkwe na watoto bima hiyo.
Aidha, Mrajisi wa Ushirika mkoani humo, Emmanuel Sanka amesema mpango huo utasaidia wanachama kunufaika na matibabu yanayotolewa na mfuko huo, hatua ambayo amedai itaongeza tija katika shughuli zao za kilimo. Mbali na hayo, Sanka amesema gharama za matibabu pasipo kutumia bima ya afya zipo juu na kuwataka viongozi wa ushirika kuwahamasisha wanachama wao kujiunga kwa wingi ili kunufaika na mpango wa serikali wa mazao matano ya kimkakati.