Shirika la taifa la hifadhi za jamii(NSSF) limeanza mchakato wa malipo ya mafao mbalimbali kwa wafanyakazi waliokosa ajira kutokana na sababu mbalimbali.
Katika taarifa iliyotolewa jana tarehe 6 januari kwa vyombo vya habari imeeleza kuanza kwa uhakiki wa majina ya madai mbalimbali ya wanachama ambao ajira zao zimekoma na walikua kwenya ajira za muda mfupi katika sekta mbalimbali kama vile madini,viwanda,ujenzi na kilimo.
Taarifa hiyo imezidi kubainisha kuwa madai yote yatakayoonekana ni halali baada ya uhakiki yatafanyiwa malipo kama ilivyokua awali.
Pia meneja wa Data na utekelezaji wa shirika hilo Cosmas Sasi amesema shirika hilo hutumia takribani sh.5 bilioni kulipa mafao ya uzeeni kwa kila mwezi ambapo mpaka sasa wastaafu 18,631 wameshalipwa.
Meneja uhusiano na Elimu wa shirika hilo aliwasihi wanachama waliositishiwa ajira zao kufika na kufanya uhakiki ambao ulianza tangu Desemba mosi 2018 na bado unaendelea katika ofisi za kanda zilizoko mikoani.
Utekelezaji wa malipo hayo kwa watu mbalimbali waliositishiwa ajira zao kwa sababu mbalimbali ni moja ya matekelezo ya agizo la Rais magufuli aliyoyatoa desemba mwaka jana katika mkutano kati yake na viongozi wa vyama vya wafanyakazi,Mamlaka ya usimamizi na udhibiti wa sekta ya hifadhi ya jamii (SSRA),watendaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii,wizara husika na chama cha waajiri.