Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko ameeleza kusikitishwa kwake na vikundi vya ujasiriamali kutorejesha mikopo kwa wakati. Mboneko amesema hayo alipotembelea na kukagua vikundi vya vijana pamoja na wanawake vilivyonufaika na mikopo ya asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani ya manispaa ya Shinyanga.
Katika maelezo yake, Mkuu huyo ameeleza kuwa, fedha hizo zinapaswa kurudishwa ndani ya muda uliopangwa kwani kwa kufanya hivyo, vikundi vingine vinaweza kupatiwa mikopo na kujikwamua kiuchumi. Mboneko ameagiza kuwa vikundi vyote ambavyo vimekuwa na matatizo kurejesha mikopo hiyo kutopatiwa tena.
“Naombeni sana vikundi ambavyo mmeshapewa mikopo mzirejeshe fedha hizo ili vikundi vingine navyo vipewe. Wale ambao wamekuwa wagumu, naagiza wasije wakapewa tena mikopo hiyo sababu tutakuwa tunateketeza fedha bure na kuipa hasara serikali. Napenda kutoa pia pongezi kwa wanawake ambao wamekuwa wakijitokeza kuunda vikundi na kufanya shuguli za ujasiriamali na kuondokana na dhana tegemezi ambayo ilikuwa ikiwasababishia manyanyaso kutoka kwa waume zao”. Amesema Mboneko.